Nane nane 2022: SUA na Teknolojia ya Uzalishaji wa Malisho ya Mifugo

Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia Idara yake ya Mashamba ya Kisasa ya Mfano, Kitengo cha Mifugo imekuja na teknolojia ya Uzalishaji wa Malisho ya Mifugo kwenye eneo dogo na kwa muda mfupi bila ya kutumia kemikali kwaajili ya usalama wa mifugo.

SUA

Akiongea na Ofisi ya Mawasiliano na Masoko, siku ya Jumatatu ya ufunguzi wa maonesho ya Nanenane tarehe 1 Agosti, 2022 Msimamazi wa Mashamba Bw. Jontas Karoli amesema ili kuzalisha mazao ya mifugo kwa wingi mfugaji anatakiwa kuwa na malisho ambayo yamezalishwa kitaalamu.

“Tumekuja kwenye Maonesho haya ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwaajili ya kuionesha jamii tena kwa vitendo kuhusiana na teknolojia ya uzalishaji wa Malisho ya Mifugo kwa kutumia eneo dogo lakini ukilitumia kiuhakika na kwa mpangilio unaweza ukazalisha zaidi”, amesema Bw. Karoli

Naye Afisa Mifugo Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama, Nyanda za Malisho na Viumbe Maji Bw. Wiliam Hozza amesema mfugaji anaweza akatumia eneo dogo kwaajili ya kuzalisha malisho ya aina mbalimbali kwaajili ya mifugo na kwa muda mfupi ambayo ndani ya wiki moja akifuata njia za kitaalamu ana uwezo wa kuvuna malisho hayo yenye virutubisho vya kutosha na kwa kutumia maji pekee kwaajili ya uzalishaji zaidi.

SUA inatoa elimu na inazalisha malisho hayo kwa njia ya kisasa ambayo haitumii udongo, mbolea wala dawa ambayo ina matumizi mazuri ya nafasi na inazalisha chakula ambacho ni salama kwa mifugo. Pia inatoa elimu ya kutosha kuhusiana na vyakula vya ziada kwaajili ya mifugo kama vile Mahindi, Mtama pamoja na Ufuta tofauti na majani kwaajili ya uzalishaji zaidi.





 

Share this page