Nane nane 2022: SUA yatoa Elimu ya matumizi endelevu ya misitu

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii imeendelea kutoa elimu kuhusiana na ukuzaji, utunzaji na matumizi endelevu ya misitu hasa upande wa vitu ambavyo vinaathiri kwa namna hasi uoto wa asili au misitu lengo likiwa kutunza uoto wa asili kwa matumizi endelevu ya misitu nchini.

SUA

Amesema hayo Afisa Misitu Mkuu na Mhadhiri kutoka SUA Bw. Stephano Kingazi wakati akiongea na ofisi ya Mawasiliano na Masoko siku ya Jumanne, tarehe 2 Agosti, 2022 katika Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Maarufu kama Nane Nane) kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro.

Aidha amesema kuwa kuna vitu mbalimbali ambavyo vinaathiri uoto wa asili iwe wa kupandwa au ule wa asili kama vile eneo lenyewe linalokuza uoto huo wa asili yaani maeneo oevu ambayo ni maeneo ya mabonde yenye majimaji ambapo ndio maeneo mkulima anayoyahitaji kwaajili ya kilimo cha Mpunga, Mahindi pamoja na kufuga na kwamba vitu hivyo vikifanywa kiholela vinachangia moja kwa moja kuharibu uoto wa asili.

“Ili mkulima aweze kuepukana na uharibifu huu wa uoto asili, mkulima anatakiwa kufanya shughuli zake katika njia sahihi, lakini pia kuepuka kuyaharibu kwa kutokata miti kiholela bila kupanda mingine na kufanya uoto wa asili kupotea,” alisema Bw. Kingazi.

SUA kupitia ndaki yake hiyo inatoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi juu ya namna nzuri ya kufanya shughuli zao lakini pia inazalisha miti ya mbao, matunda, vivuli na mapambo ambayo inaweza kupandwa katika maeneo yetu na kusaidia kueneza uoto wa asili. 

 

Share this page