Serikali kushirikiana na SUA kutunza eneo la Utalii wa Kihistoria

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema serikali kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuyaendeleza, kukarabati na kutunza kumbukumbu zote za kihisitoria  zilizoachwa na wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini katika eneo la Kampasi ya Solomon Mahlangu.

Serikali kushirikiana na SUA kutunza eneo la Utalii wa Kihistoria

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (kushoto) akiwasili katika Kampasi ya Solomon Mahlangu, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando na kulia Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi Dkt. Geoffrey Karugila

Mhe. Gekul ameyasema Januari 18, 2022 mjini Morogoro wakati alipotembelea  makaburi 97 ya wapigania uhuru wa chama cha ANC cha Afrika ya Kusini yaliyoko Kampasi ya Solomon Mahlangu na yanatunzwa na SUA kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo amesema mali kale na kumbukumbu zote za kihisitoria zinapaswa kutunzwa  vizuri ili vizazi vya sasa na  baadae viweze kutambua  historia za nchi zao.

“Tutayatangaza tukishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii yawe ni maeneo ya vivutio  ya kiutalii  wa kihistoria  kwa wenzetu ambao wanapenda kupata historia za nchi zao,  lakini pia na watalii wengine  wafike kwenye maeneo haya kwa hiyo tuko hapa  kwa ajili ya kazi hiyo na lengo ni kushirikiana na hizo nchi  kwa ukaribu ili tuone na wao wanashirikije katika kutunza  historia hii” amesema Gekul

002

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akisikiliza maelezo kutoka kwa Bw. Ali Mkopi mtumishi wa SUA anayelijua vizuri eneo hilo la Makaburi ya Wapigania Uhuru wa ANC

Aidha ameongeza kuwa kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na SUA kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inapaswa kutambua watoto na mama wa familia za wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini ili nao wawe sehemu ya historia pale zinapokuja familia zao kutoka Nchi ya Afrika ya Kusini.

Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Bw.  Boniface Kadili amesema eneo la Mazimbu  ni sehemu moja wapo ya  Ukombozi wa Bara la Afrika   na jitihada zilizopo  kwa sasa kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ni  kulitangaza katika gazeti la Serikali ili  eneo hilo liweze kuwa katika Ulithi wa Taifa.

“Eneo hili likishalindwa kisheria  sio kwamba linakuwa ni miliki ya  Maliasili au  Wizara yetu  bado litaendelea kuwa miliki ya SUA ila sisi tunachofanya  ni kutoa ushauri wa kitaalamu  wa kuhifadhi eneo ili muhimu. Amesema Boniface Kadili Mratibu wa Kituo cha Urithi  wa Ukombozi wa Bara la Afrika “ amesema Gekul

Aidha Mhe. Gekul ameagiza Afisa Utamaduni Mkoa wa Morogoro na Afisa Utamaduni Manispaa ya Morogoro kuhakikisha wanatambua maeneo yote ya kihistoria  ya asili  ndani ya maneo yao ili kumbukumbu hizo zitumike kwenye historia ya Tanzania.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando amesema katika wilaya ya Morogoro yapo maeneo mengi  ya kihistoria ya asili ambayo  yanapaswa kutunzwa  lakini changamoto kubwa iliyopo kwa sasa  ni ukosefu wa watu ambao wanaweza kutunza maeneo hayo hasa yanayohusu  Machifu waliofia katika wilaya ya Morogoro.

003

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando (aliyevaa suti)

Akitoa taarifa ya namna ambayo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kilivyopewa majengo na maeneo hayo ya Kampasi ya Solomon Mahlangu  kutoka kwa wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi, Dkt. Geoffrey Karugila  amesema kambi hiyo ilianzishwa mwaka 1978 lengo likiwa ni kupigania uhuru wa Nchi ya Afrika ya kusini kupitia Chama cha ANC.

Dkt. Geoffrey Karugila   ameendelea na kusema mwaka 1999 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikabidhi eneo hilo rasmi kwa SUA ambapo  mwezi Machi mwaka 1999 Baraza la Chuo liliamua kubadilisha  jina  kutoka SUMAFUCO na kuliita Kampasi ya Solomon Mahlangu na lina miundombinu mbalimbali iliyoachwa ikiwemo Madarasa, Hospitali  na Jengo la Utawala.

004

 

Share this page