Serikali na SUA wadhamiria dawa asili kuvuka mipaka ya Tanzania

Katika kuhakikisha Waganga wengi wa tiba asili nchini wanauza dawa bora na salama kwa binadamu, wanyama na mazingira, Mkemia Mkuu wa Serikali amepunguza gharama za upimaji wa dawa hizo ili zipimwe na kusajiliwa kisheria.

SUA

Meneja wa maabara ya chakula na dawa kutoka Mamlaka ya maabara ya Mkemia mkuu wa Serikali Dkt. Shimo Peter wakati akizungumza na waganga wa tiba asili kwenye warsha ya wadau wa tiba asili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania

Hayo yamebainishwa na Meneja wa maabara ya chakula na dawa kutoka Mamlaka ya maabara ya Mkemia mkuu wa Serikali Dkt. Shimo Peter wakati akizungumza na waganga wa tiba asili kwenye warsha ya wadau wa tiba asili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania iliyoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia mradi wake wa Valorization of potentials of Synadenium glaucescens (SG) Phytochemicals for Management of Important Human and Animal diseases (VaSPHARD)

“Kumekuwa na maombi ya muda mrefu ya waganga wa tiba asili kuomba Mkemia Mkuu wa Serikali kupunguza gharama za upimaji wa dawa ili waweze kusajiliwa, kwahiyo mkemia mkuu ameliangalia na hatimae amepunguza gharama kutoka dola za kimarekani 311 hadi kufikia dola 152 ambayo ni karibu nusu ya gharama za awali” alisema Dkt. Shimo

Amefafanua kuwa ili kuweza kupimiwa kwa kutumia punguzo hilo kuna taratibu ambazo wanapaswa kuzifuata ikiwemo kujaza fomu kutoka baraza la tiba asili na tiba mbadala au waratibu wa tiba asili kutoka wilayani au mkoani na kwamba kinyume na hapo watajikuta wanalipa zaidi ya dola 500 kwa dawa moja.
Amewataka kufikisha taarifa hizo kwa wenzao kote nchini ili waweze kutumia fursa hiyo ambayo wame iomba kwa muda mrefu ili waweze kuuza dawa zenye viwango na ubora utakaowawezesha kufikia soko la ndani na la nje ya nchi.

Amewasisitiza watoa huduma kuzalisha dawa asili kufuata kanuni na miongozo ya uzalishaji bora na salama kutumia kemikali kufuata sheria ya kemikali namba 3 ya mwaka 2003 inayosimamiwa na GCLA na kupata mafunzo ili kuweza kutambua njia salama za matumizi ya kemikali.

Dkt. Faith Mabiki akielezea lengo la warsha hiyo

Awali Mkuu wa Mradi wa GRILL na VaSHPARD kutoka SUA Dkt. Faith Mabiki amesema lengo la warsha hiyo ni kuendeleza jitihada za Chuo na Serikali katika kubadili tabia za namna wanavyotengeneza dawa za asili na wanavyotoa huduma kwa jamii.

“Kwa kuwa toka tumeanza mradi tumeona mabadiliko makubwa sana katika utengenezaji wenu wa dawa na utoaji wenu wa huduma hivyo tunaamini warsha kama hii inayowakusanyisha pamoja kutoka mikoa mbalimbali na kupata mafunzo kutawasaidia zaidi kutoka kwenye kufanya kazi kwa mazoea kwa kubadili tabia na hatimae kutengeneza dawa asili zenye viwango vinavyokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi” alieleza Dkt. Mabiki

Mtafiti huyo amesema kwenye warsha hiyo pia watatoa matokeo ya vipimo vya dawa zao mbalimbali walizozipeleka SUA kwaajili ya vipimo zilizobaki kutoka kwa  Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye aliomba wataalamu wa SUA kusaidia kuzipima na kuwapatia majibu kila mmoja na kumshauri mambo ya kufanya ili kufikia ubora unaotakiwa.

Amesema dawa kutoka nje ya nchi tunazoziona zinapitia michakato mingi ili kuweza kupata nembo za ubora na mamlaka za nchi hizo na kimataifa ndio maana SUA na Serikali kupitia mkemia mkuu wa serikali wanashirikiana ili kuwawezesha waganga hao waweze kufikia soko kirahisi la nje.

Amewataka kuendelea kushirikiana miongoni mwao na kuwasiliana katika masuala mbalimbali kwakuwa kila mmoja ana uelewa tofauti kutokana na mazingira wanayotoka na itawasaidia kupeana ujuzi na kuongeza uelewa zaidi badala ya kila mmoja kufanya mambo yake kwa siri.

Akizungumza kwa niaba ya waganga wengine walioshiriki warsha hiyo Dkt.Flavian Nyakeji kutoka Njombe amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kusikia kilio cha gharama kubwa za upimaji wa dawa na kuahidi kuitumia fursa hiyo vyema ili kuweza kufikia viwango.

“Swala la gharama kubwa za upimaji limekuwa kilio chetu cha muda mrefu maana wengi wetu kweli tunazo dawa za asili nzuri na zinatibu lakini hatuna uwezo wa kulipa dola 500 na zaidi kupima dawa moja ili tusajiliwe  lakini sasa kwa gharama hiyo ya shilingi dola 152 tutahakikisha tunapima dawa zetu  kwa faida yetu, jamii na wateja wetu” alisema Dkt.Nyakeji

Katika warsha hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo,aina za kemikali kwenye mimea, Utengenezaji wa kemikali, kazi za kemikali kwenye mimea na utabibu, athari za sumu kuvu katika afya na biashara, namna ya kupunguza na kuzuia sumu kuvu kwenye kwenye bidhaa, Matatizo ya kiafya yanayosababishwa na vimelea, mambo hatari yanayochangia kuwepo kwa vimelea pamoja na mada zingine nyingi.

Warsha hiyo ilifanyika siku ya Jumatano tarehe 11 Mei 2022 mkoani Morogoro na kuwakutanisha waganga wa tiba asili kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania hususani wale ambao walipeleka dawa zao kwa mkemia mkuu wa serikali kwaajili ya vipimo na zikabaki ili waweze kupewa majibu ya dawa zao.

Mkemia Dkt. Richard Madege akitoa matokeo ya majibu ya vipimo vya dawa zilizopimwa katika maabara ya SUA kuangalia ubora wa dawa hizo zinazozalishwa na waganga wa tiba asili

Prof. Robinson Mdegela akifundisha kuhusu madhara ya vimelea tajwa kwa afya ya binadamu na akifafanua matokeo ya utafiti ya sampuli hizo za dawa kwa ujumla wake



Waganga wa tiba asili kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania wakifuatilia kwa makini matokeo ya vipimo vya dawa zao yaliyofanywa na Maabara za SUA

Habari na Picha: Calvin Gwabara - SUAMEDIA

Share this page