SUA kuchangia CHAHITA ili kuboresha elimu ya Hisabati

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeahidi kutoa kiasi cha sh. 1,000,000/= kila Mwaka kwa ajili ya kukiunga mkono Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA)  katika harakati wanazozifanya kwa ajili ya kuboresha Elimu ya Hisabati nchini ikiwemo utoaji wa Mafunzo kwa Walimu wa Hisabati.

Profesa Raphael Chibunda

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Warsha ya 56 ya Kitaifa ya Hisabati Tanzania na Mkutano Mkuu wa Chama uliofanyika Kampasi ya Solomon Mahlangu SUA.

Amesema CHAHITA kinahitaji angalau Sekta ya Umma ili kukipa nguvu katika kushawishi Walimu wa Somo la Hisabati kuhudhuria Warsha mbalimbali zinazotoa mafunzo katika kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji hivyo atashirikiana bega kwa bega na Uongozi wa Chama hicho ili kuona wanachoweza kufanya katika kuishawishi Wizara ya Elimu lakini kuishawishi TAMISEMI katika kusaidia chama hicho kwenye shughuli zake.

Prof. Chibunda amesema Uongozi wa Chama unafanya kazi kubwa sana katika kutatua hali mbaya ya ufaulu kwenye somo la Hisabati lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwemo kujenga uelewa kwa jamii kuhusiana na somo hilo.

“Wanahesabu hawa ni wa muhimu sana lakini ujuzi wa hesabu walionao hauwapi wadau kama walivyo Wahandisi na Wakandarasi kushawishika kwamba hii kampuni bila Hesabu isingesimama inaweza kutuchukua muda kwa hiyo tutahitaji “intervation” ya angalau Sekta ya kiserikali kuweza kusaidia hasa pande za pembezoni ambapo kuna shida kubwa katika somo hili la hesabu hivyo tunahitaji nguvu ili walimu wa Hesabu kutoka maeneo yote ya Tanzania kuhudhuria Warsha kama hizi” , amesema Prof. Chibunda


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) Bi. Betinasia Manyama amesema changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na ufaulu hafifu wa somo la hisabati hasa kwa ngazi ya Msingi na Sekondari ambapo kunachangiwa  hasa na upungufu wa walimu kwa ngazi zote za Elimu ambapo wameelemewa na idadi kubwa ya vipindi.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa Fedha za kuendeshea kazi mbalimbali ndani ya chama ikiwemo nauli kwaajili ya kuwapatia waalimu kwenda kufundishia mwezi wa tatu kila mwaka pamoja na Walimu wa Hisabati kukosa Hamasa kutokana na kazi nyingi huku Mshahara ukiwa ni uleule kwa walimu wote bila kujali mwalimu wa somo hili ana vipindi vingi na somo lake linahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu.

“Wastani wa waliofaulu katika miaka tisa iliyopita katika mtihani wa Hisabati wa kitaifa kwa shule za msingi ni asilimia 31.86 na katika shule za sekondari ni asilimia 76.46, kwa mfano ufaulu wa Hisabati kwa kidato cha nne mwaka 2021 ni 19.54% hivyo ni vyema Serikali kulipa somo la Hisabati umuhimu maalum maana ndio nguzo ya masomo yote hasa masomo ya Sayansi na pia bila Hisabati hakuna Wahandisi na hivyo hakuna Viwanda”, amesema Bi. Betinasia Manyama.


                                                       
 

Share this page