Kuanzia tarehe 7 hadi 27 Oktoba 2021, Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kiliandaa na kuendesha mafunzo maalum ya ubunifu wa mavazi kwa wajasiriamali mbalimbali wanaojishughulisha na ubunifu wa mavazi wa mkoa wa Morogoro.
Washiriki wote waliobahatika kuhudhuria mafunzo hayo walipatiwa ujuzi na maarifa mbalimbali ya Ubunifu wa Mavazi kama vile Kanuni za Maumbo ya Mwili na Nyuso katika Kuandaa mavazi, biashara ya mavazi, pamoja na kanuni na mbinu za huduma kwa wateja.
Katika siku ya mwisho ya kuhitimisha mafunzo hayo, wahitimu hao walitakiwa kuyatumia mafunzo waliyoyapata vizuri ili kuweza kuwasaidia katika kazi zao pamoja na kuonesha mabadiliko na tofauti kwa mafundi wengine ambao bado hawajapokea mafunzo hayo.
Akizungumza katika tukio hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Uzamili,Utafiti ,Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo, Mratibu wa kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Doreen Ndosi amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya wahitimu hao kuwaambukiza ubunifu watu wengine ili kuhakikisha wabunifu wengi wanaelimika ili kuweza kwenda sawa na soko la biashara zao.
Mgeni rasmi Dkt. Doreen Ndosi akikabidhi cheti kwa mmoja wa wabunifu Bi Asha Kapagala
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi ambaye pia ni Mwalimu wa Mafunzo hayo, Bw. Valentino Mwinuka amewataka wahitimu hao wafuate taratibu na kanuni za ufundi na waende na wakati pamoja na kuwa waaminifu katika kazi zao ili kuweza kujitengenezea soko lililo bora katika shughuli zao.
“Mkawe waaminifu na kuwa tayari kujifunza sehemu mbalimnali, msikae tu sehemu moja mkashindwa kuwatembelea hata mafundi wenzenu ama kusafiri kwenda kuhudhuria maonesho mbalimbali kama vile Sabasaba na Nanenane, hata kama hamna bidhaa kusafiri kwenda kwenye maonesho kutawaongezea tija katika kazi yenu”, amesema Bw. Mwinuka.
Wabunifu wa mavazi wakisikiliza nasaha za mgeni rasmi
Aidha Mwenyekiti wa Kongano la Nguo Manipaa ya Morogoro Bw. Robert Mathias amewashukuru SUA kwa kuandaa mafunzo hayo na kutaka kuendelea kushirikiana nao ili kuweza kutengeneza wabunifu zaidi Mkoani Morogoro.
Naye mmoja wa wabunifu wa mavazi aliyebahatika kupata mafunzo hayo kutoka SUA, Bi. Herieth Mbwambo amewataka wabunifu wengine kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajenge utaratibu wa kukimbilia fursa zinazotokea ili waweze kujifunza kuendana na soko linavyokwenda.
Aidha Willy Mbuma mmoja wa wahitimu amesema kuwa mafunzo hayo yatabadilisha vipato vyao lakini pia na jamii inayowazunguka huku uchumi wa nchi ukiendekea kukua kadri wanavyozidi kupata manufaa zaidi.
“Wawe wanaandaa mafunzo haya mara kwa mara na yawe endelevu ili na watu wengine waweze nao kupata elimu hii ambayo sisi tumeipata kwa kuwa hawawezi kwenda mbele zaidi kama hawajaipata elimu hii ambayo sisi tumeipata”, amesema Bw. Mbuma.
Soma pia
SUA yawanoa wabunifu wa mavazi kuinua uchumi wa viwanda vidogo
Story & Photo Credits
Amina Hesron - SUAMEDIA