SUA yatoa mafunzo ya ukamataji wa wanyama pori katika hifadhi ya Tarangire

Katika kuhakikisha wanapatikana Wataalam waliobobea katika uhifadhi Wanyama Pori, Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA kimetoa mafunzo kwa vitendo kwa Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza wanaosoma Kozi ya Uhifadhi Wanyama Pori katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire iliyopo Mkoani Manyara.

SUA

Akizungumzia mafunzo hayo, Dkt. Richard Samson Joachim  kutoka Idara ya Upasuaji na Uzalishaji Wanyama  iliyopo  Ndaki ya Tiba ya Mifugo na Sayansi Shirikishi  SUA  amesema nia kubwa ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Wanafunzi  kuwa karibu na Wanyama Pori pamoja na kuhakikisha usalama wao pamoja na wanyama unakuwepo kwa kuwapa mbinu sahihi za kuwakamata wanyama hao.

‘‘Nia kubwa ya mafunzo haya kwa vitendo ni kuwajengea uwezo wa kuwa karibu na WanyamaPori kujifunza jinsi gani unaweza kutunza Wanyama Pori lakini vile vile kuhakikisha kwamba usalama wako wewe na usalama wa mnyama unakuwepo,  tulikuwa na shughuli nyingi kama kukamata wanyama  tulifanikiwa kuwakamata wanyama  kadhaa kama Pundamilia, Nyumbu, Simba na Tembo’’, amesema Dkt. Richard

Naye Afisa Muhifadhi kutoka hifadhi hiyo ya Tarangire kitengo cha Tiba ya Wanyama Godwin Olomi amesema kuwa wamewapokea wanafunzi hao na kuwapa maelezo kuhusiana na tahadhari katika maeneo ya kukamatia wanyama na nini cha kufanya baaada ya mnyama kukamatwa akiwa chini.

“Wanafunzi tumewapokea na tumewapa maelekezo vizuri na wamefuata maelekezo na wamepata kitu kwa sababu tunategemea wao ndio wahifadhi na wengine watakuja kusimamia hata vitengo hivi, kwa hiyo wanatakiwa wafahamu hata vitendo vinavyofanyika ili kusudi huko mbeleni na wao waje kufanya haya mambo”, amesema Olomi.

Ameongeza kuwa wao kama Hifadhi ya Taifa ya Tarangire wanatarajia kile ambacho wamewaelekeza wanafunzi hao kuja kukifanyia kazi vizuri hata katika hifadhi zingine zilizopo nchini na pia ameendelea kuwakaribisha wanafunzi kuendelea kwenda kujifunza kwa sababu wanyama wanaopatikana ni wengi na hivyo wanafunzi hao watajifunza na kupata mengi kuhusiana na uhifadhi Wanyama Pori.

Kwa upande wa Wanafunzi akiwemo Nyalugobi Mkama kutoka kozi hiyo amesema kupitia mafunzo hayo wameweza kujifunza vitu mbalimbali na kuwafungua macho zaidi hata kwa vile ambavyo walikuwa hawavitambui ikiwemo kukamata wanyama wadogo pamoja na wakubwa na wale waishio majini.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewafanya kuwa bora zaidi na yatawawezesha kufanya kazi zenye ubora na tija kwa jamii ambayo ndio  walengwa kwa huduma zao.

Naye Joel Maganga amesema kuwa mafunzo hayo ya kukamata wanyama kwa kutumia vifaa mbalimbali, kutibu wanyama ambao wamepata matatizo, namna ya kutofautisha wanyama kwa jinsia zao pamoja na kujua namna uoto wa hifadhi unavyotunzwa ili kuwafanya wanyama wawe salama umewafanya wao kama Wanafunzi na wafanyakazi wa hapo baadae kufanya kazi zao kwa utaalam zaidi kwa maendeleo ya nchi.

Mafunzo hayo kwa vitendo yalifanyika kuanzia tarehe 7 Juni hadi 05 Julai 2022.

Imeandikwa na Gojo Mohamed - SUAMEDIA

Share this page