Tathlitha ya kumi na mbili ya Baraza

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Mwenyekiti wa Baraza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman pamoja na wajumbe wote kwa kazi Kubwa na nzuri waliyoifanya na ushirikiano waliouonesha katika kusaidia mafanikio ya Chuo na utekelezaji wa majukumu ya Chuo kwa ufanisi.

SUA

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo Mhe.Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman wa katikati (waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza

Shukrani hizo amezitoa wakati wa Mkutano wa “167” wa Baraza uliofanyika siku ya Alhamisi tarehe 23 Juni 2022, katika ukumbi wa Baraza wa Chuo na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza pamoja na wajumbe wengine wa baraza hilo.

Kwa upande wake Bi. Maryam J. Saadalla Mjumbe kutoka Wizara ya Kilimo Zanzibar ambaye anamaliza kipindi chake ameishukuru Menejimenti ya Chuo kwa kazi nzuri waliyoifanya pamoja na mafanikio makubwa yaliyofanyika kwa kipindi chote alichokuwa katika baraza hilo Ikiwemo Chuo kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Katika mkutano huo Baraza imetoa taarifa ya kumaliza tathlitha ya kumi na mbili ya Chuo pamoja na muktasari wa utekelezaji wa majukumu katika Chuo hicho. 

Akilezea utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika tathlitha ya kumi na mbili, Chuo kimefanikiwa kufanya maswala mbalimbali ikiwemo kuidhinishwa kwa Muundo mpya wa Chuo ili kuongeza tija na kukiandaa Chuo kupanuka na kuongeza idadi ya wanafunzi. Vile vile Chuo kimeweza kufanya vizuri katika Nyanja za Tafiti kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Pia Baraza limechangia kwa kukiwezesha Chuo kupanua shughuli zake kwa kujenga Maabara Mtambuka na kufungua Kampasi mpya ya Mizengo Pinda, vituo vya Mafunzo na Mashamba Darasa katika baadhi ya Mikoa ili kufundisha wakulima kuhusu kilimo na kilimo biashara kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Baraza la Chuo limeundwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Vyuo Vikuu sura ya 346 ya Sheria za Tanzania ikisomwa pamoja na Ibara ya 18 ya Hati Idhini ya SUA,2007.
 

Share this page