Viwavijeshi Vamizi (fall armyworm) ni wadudu hatari kutoka barani Amerika ambao waliingia Afrika mwaka 2016 na kufika Tanzania mwaka 2017. Wadudu hawa wanashambulia mazao zaidi ya 80 lakini chakula chao kikuu ni zao la Mahindi ambayo pia ndio chakula kikuu cha Wanzania.
Wadudu hawa wamesambaa kwa sasa kwenye zaidi ya mikoa 15 na wameleta athari kubwa kwa wakulima wa mahindi na sasa mahindi yanapokauka wanakula Pamba, Mihogo na mazao mengine ya biashara na chakula hali ambayo inawafanya wakulima kupata shaka na wasiwasi wa usalama wa chakula.
Barani Amerika ambako mdudu huyu alianzia wao wamemkabili kwa kuzalisha mbegu zilizozalishwa kwa teknolojia ya Uhandisi jeni yaani Genetic Modification (GM) na kupata mbegu za GMO ambazo zina sifa ya kumkabili mdudu huyu kwa kuupa mmea sifa yaani Gene au Jeni ambayo mdudu huyu akila anakufa na akinusa Jeni hiyo hawezi kushambulia.
Hapa nchini kwetu Serikali kupitia wizara ya kilimo imetoa maelekezo na madawa ya kumkabili mdudu huyu lakini wakulima wengi wanalalamika kuwa dawa hizo hazimuui na pengine hii ni kutokana na kula na kujificha kwenye kiini cha mhindi.
Bado wakulima wengi hawawafahamu wadudu hawa na mazao yao yanaendelea kushambuliwa hadi sasa hivyo makala hii ambayo imetayarishwa kwanjia ya video inalenga kutoa uelewa kuhusu mdudu huyo na mbinu za kukabiliana nae.
Hapa utawasikia wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wakimzungumzia namna wanavyomfahamu mdudu huyu na athari anazoleta pamoja na mbinu ambazo serikali na watafiti wanazichukua katika kumkabili.
Makala hii imetayarishwa na Calvin Gwabara, Mwandishi wa habari Mwandamizi katika masuala ya kilimo kutoka Vyombo vya habari vya Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA yaani SUAMEDIA.