Wafanyakazi SUA wahimizwa kujikinga dhidi ya maambukizi ya Corona

Madaktari, Wauguzi na wafanyakazi wengine wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kutokupuuza na kuchukua tahadhari zote zinazohitajika ili kujikinga na kupata maambukizo ya Virusi vya Corona na kuepuka kuambukiza wengine wakati wa utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo.
 

COVID-19

Baadhi ya watumishi wa Idara ya huduma za hospitali ya SUA wakiwemo madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wakimsikiliza Dkt. Omar Kasuwi wakati akifungua mafunzo hayo

Wito huo umetolewa na Daktari Mkazi wa Hospitali ya SUA, Dkt. Omar Kasuwi wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wote wa Idara ya huduma za hospitali yaliyofanyika hivi karibuni katika kampasi ya Solomoni Mahalangu Mazimbu.

Dkt. Kasuwi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa na uwezo watumishi wa hospitali hiyo kama sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo tishio kwa sasa duniani kutokana na kuua watu wengi, kusambaa kwa kasi duniani  pamoja na kukosa kinga wala dawa kwa sasa.

Sote tunafahamu juu ya uwepo wa janga hili kubwa la ugonjwa wa Corona duniani na pia tunafahamu namna ambavyo serikali na Chuo chetu kinavyopambana kuhakikisha watumishi na wanajumuiya wa SUA hawapati maambukizi na nyinyi kama watoa huduma za afya mpo kwenye hatari kwakuwa mnahudumia wagonjwa na mnaweza kuambukizwa na kuambukiza pale mtakapokutana na mgonjwa mwenye maambukizi wakati wa kumhudumia bila kujua - Alifafanua Dkt. Kasuwi.

Amefafanua kuwa kwa kutambua mazingira ya watoa huduma za afya, Chuo kimeamua kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ya kuwajengea uelewa juu ya ugonjwa huo chanzo chake, Unavyoweza kuambukiza na namna ya kujikinga ili iwe rahisi kuukabili endapo utatokea chuoni kwetu.
 

COVID-19

Kiongozi wa hospitali ya SUA na Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo Dkt. Omar Kasuwi (Wa Pili kushoto) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa kundi la pili la wafanyakazi wa Idara ya huduma za hospitali.

Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  SUA, kilianza kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuingia kwa virus hivyo nchini ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya kushauri Chuo juu ya virusi vya corona ,uhamasishaji wa matumizi ya  vimiminika  vya mikono kwa nyakati zote watumishi wawapo ofisini na majumbani na maboresho katika hospitali ya SUA  ikiwemo hiyo ya kutoa elimu kwa wahudumu wa afya.
 

COVID-19


Wakati dunia ikishuhudia kuendelea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona, Daktari  Kasuwi ametoa wito kwa wanajumuhiya wa SUA  na Watanzania kwa ujumla  kujifunza kubadili tabia, Kusikiliza na kufuata malekezo ya kitaalamu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo  na kuacha mazoea hasa katika masuala yanayogharimu maisha ya watu. 

Lazima  tahadhari za pamoja za afya zifuatwe na kila mmoja anatakiwa kujilinda na kulinda mwingine na jamii kwa ujumla kwa kuwa uzembe kwa mtu mmoja unaweza kuambukiza jamii na kueneza virus hivyo kupelekea kugharimu maisha ya watu kama tunavyoona huko nchini Italia, China na zingine nyingi -Alibainisha Dkt Omar Kasuwi.

Dkt. Kasuwi amesema mpaka sasa Dunia haijapata dawa wala chanjo ya virusi vya corona tangu  kugundulika kwake nchini china mwishoni mwa mwaka 2019
 

COVID-19Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika hospitali ya SUA na Dakatari kiongozi wa hospitali ya SUA upande wa Mazimbu Dkt. Elimwidimi Swai akiwasilisha mada yake juu ya ugonjwa huo

 

 

 

Like & Share this page