Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamekaribishwa rasmi huku wakihimizwa kutumia vizuri rasilimali zilizopo Chuoni hapa ili wajifunze kwa vitendo kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda wakati wa kuhitimisha wiki ya kuwakaribisha wanafunzi na kuyatambua mazingira ya Chuo kwa wanafunzi wapya wa mwaka wa masomo 2021/2022 yaliyofanyika Siku ya Ijumaa tarehe 29 Oktoba 2021 katika ukumbi wa Solomon Mahlangu Freedom Square uliopo Kampasi ya Solomon Mahlangu.
“SUA kazi yetu kubwa tuliyonayo kwenu ni kuwafanya mjifunze kwa vitendo hivyo tumieni vyema rasilimali za chuo ipasavyo, kama unatakiwa uende maabara ya TEHAMA, shambani, Hospitali ya wanyama na karakana nenda kajifunze kwani sehemu hizo ziliandaliwa ili mjifunze kwa vitendo” alisema Prof. Mwatawala
Prof. Mwatawala amesema kuwa lengo la Chuo ni kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo ili kuwaandaa kujiajiri pamoja na kujitegemea waweze kusaidia jamii na kuleta maendeleo nchini.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Maulid Mwatawala akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza.
Amesema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza walifanya uchaguzi sahihi wa kuchagua SUA kwani chuo kina ubora wa hali ya juu na kinafundisha kwa vitendo na kinaongoza kutoa tafiti nzuri nchini pia kina mazingira mazuri ya kusomea na kujifunza vitu mbalimbali.
“Ukifeli ni wewe umeamua kufeli kwani Chuo hiki kina mazingira mazuri ya kukufanya usome na ufaulu hata ukiamua kuburudika kidogo unaweza kusikiliza Redio yetu ya SUA itakufanya uchangamshe akili” alisema Prof. Mwatawala
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Utawala na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa amesema kuwa lengo la kuaanda zoezi hilo ni kuwafanya wanafunzi hao wayajue mazingira , kutambua viongozi wa Chuo na sheria mbalimbali zilizowekwa Chuoni hapo.
Prof. Muhairwa amewashauri wanafunzi hao kutumia muda wao vizuri wanapokuwa Chuoni kwani elimu ya SUA sio ya kucheza bali wasome kwa bidii ili kutimiza malengo yao pia wasome vitu mbalimbali kwenye SUA Websites watajifunza vingi.
Aidha amewataka wawe wawazi wanapokutana na changamoto yoyote ile iwe ya kifamilia, mahusiano, ugonjwa hata kama ni unyanyasi wa kijinsia wasikae kimya waende ofisi za ushauri wapate msaada kuliko kubaki nazo zikawatesa.
“Hakuna aliye juu ya sheria kama hujafanyiwa kitu sahihi toa taarifa hasa nyinyi wasichana usikubali kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia ukanyamaza kimya, yani usivumilie tatizo wakati sehemu za kukusaidia zipo” Alisema Prof. Muhairwa.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa mwaka wa masomo 2021/2022
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii na Insia kutoka SUA Prof. Samweli Kabote amewapongeza sana wanafunzi hao kwa kuchaguliwa na kuichagua SUA kwani elimu inayotolewa hapa ni ya tofauti ukilinganisha na Vyuo vingine na inamuandaa muhitimu kujiajiri.
Pia amewataka wanafunzi hao kutumia Lugha ya Kingereza muda wote sababu masomo yao yameandikwa kwa Lugha hiyo, wapende kuongea kingereza itawasaidia kuelewa masomo yao na vitu vingine.
“Wanafunzi wengi wakishafika Chuo hawapendelei kuongea lugha ya kingereza lakini ukweli ni kwamba masomo mengi Chuoni hapa yanatumia lugha ya kingereza hivyo itumieni na muipende” alisema Prof. Kabote.
Ameongezea kwa kuwataka kuepuka vishawishi, kutokuiga maisha ya mtu mwingine bali kuzingatia masomo yao na kujifunza vitu ambavyo vitawasaidia katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake, Mshauri wa wanafunzi Bw. Pule Motshabi amewapongeza wanafunzi hao kwa kuchaguliwa SUA na kuwahakikishia kuwa wamefanya chaguo sahihi.
Amesema kuwa Chuo kimejipanga vizuri kuwafundisha na kimeboresha miundo mbinu ya kufundishia ili kuhakikisha kile walichotegemea kukipata chuoni hapo wakipate kwa vitendo zaidi.
“SUA sio sehemu ya kugawa vyeti tu bila kuonyesha juhudi ya kusoma kwa bidii ili upate cheti hicho wala elimu ya hapa sio rahisi ila tumejipanga kuwasaidia na kuwashauri mfanye vizuri kwenye masomo yenu” alisema Bw. Motshabi.
Mshauri wa Wanafunzi, Bw. Pule Motshabi
Story and Photo Credits
Amina Hesron & Calista Nyimbo - Communication & Marketing, SUA