Wanasayansi watakiwa kufanya tafiti zinazotatua matatizo ya jamii na zilenge mapinduzi ya nne ya viwanda yajayo

Wanasayansi wanaochipukia katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wametakiwa kuhakikisha wanaandika maandiko ya Utafiti ambao utaalenga kutatua matatizo ya jamii moja kwa moja bila kusahau tafiti ambazo zinaweza kuisaidia nchi kufikia mapinduzi ya nne ya viwanda.

SUA

Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha hiyo pamoja na viongozi wa Chuo

Ushauri huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma utafiti na ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa wanataaluma wachanga wa Chuo hicho juu ya namna ya kuandika maandiko kwaajili ya kuomba fedha za kufanya tafiti.

“Tusifanye tafiti kwaajili ya kupanda madaraja au vyeo kwenye kazi zetu bali tufanye tafiti ambazo zinaweza kwenda kujibu changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi na Jamii yetu, kwa namna hiyo ndio mtakuwa mmefikia lengo hasa la kufanya utafiti” Alieleza Prof. Mwatawala.

Aidha amesema amepitia baadhi ya maandiko yaliyoafanywa na baadhi yao ameona yamegusa kwenye maeneo mbalimbali kama vile tafiti za Bioteknolojia, Roboti na maeneo mengine muhimu maana huko ndiko dunia inakoelekea katika mapinduzi ya nne ya viwanda.

“Kuna mambo mengi makubwa ambayo yanakua kwa kasi sana duniani kwa sasa kuelekea mapinduzi ya nne ya Viwanda, nyinyi kama wanasayansi hakikisheni mnafanya tafiti hizo nchi yetu pia isibaki nyuma ili pale mambo hayo ili itakapofika nchini kwetu tuwe tayari na uelewa mpana na kuingia bila woga na sisi kunufaika” Alisisitiza Prof. Mwatawala.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma utafiti na ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala (aliyesimama) Akifungua warsha hiyo

Naibu makamu huyo wa Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na ushauri wa kitaalamu amesema Uongozi wa Chuo mwaka jana umetoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwaajili ya kufadhili maandiko ya tafiti za Wanasayansi wanchanga Chuoni hapo na mwaka huu wameongeza kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1 ili kuongeza wigo na fursa zaidi kwa Wanataaluma wake kujifunza.

“Kwa mchanganyiko huu ninaouona humu ndani jinsi ulivyowakilisha Ndaki na idara mbalimbali na kampasi zetu ninaamini mpango huu utawafanya na kukifanya Chuo kudumu kwa miaka 30 zaidi na kukipandisha Chou kwenye tafiti za Sayansi na ubora dunaini” Alisisitiza Prof. Mwatawala.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo Naibu makamu Mkuu wa Chuo Utawala fedha na miapango Prof. Amandus Muhaurwa amewataka Wanasayansi hao wachanga kuhakikisha wanafuata taratibu katika utekelezaji wa kazi za tafiti zao pale wanapopata ili kuondoa mikwamo isiyo na lazima.

“Unapoona unahitaji fedha kwenda field kukusanya data au taarifa ni vyema ukaleta maombi wiki moja kabla au zaidi hii itasaidia sana maombi yako kufanyiwa kazi haraka na hivyo kuweza kupata fedha mapema na kutekeleza majukumu yako kwa wakati na hii itasaidia kufikia malengo yenu.” Alieleza Prof. Muhairwa.

 Amewataka kufanya tafiti zao kwa weledi ili waweze kulisaidia taifa na kuepuka misuguano mbalimbali ambayo itasababisha kupata taarifa zinazokanganya ambazo mwisho wa siku anaamini wengi huaishia kwenye kupika taarifa kitu ambacho sio sahihi kisayansi.

Naibu makamu Mkuu wa Chuo Utawala fedha na miapango Prof. Amandus Muhaurwa akita neno kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shahada za Juu Utafiti na Ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Karimuribo ameushukuru uongozi wa Chuo kwa kuamua kutenga fedha zake za ndani kwaajili ya kufadhili tafiti za wanataaluma wake ili kukuza uwezo wao kuingia kwenye utafutaji wa fedha kubwa za utafiti dunaini.

“Nimatumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya na Uongozi wa Chuo unavyotoa fedha utasaidia Chuo chetu kitaongoza kwa kupata fedha nyingi za miradi ya utafiti nchini na hivyo kuchangia zaidi kwenye kutafuta ufumbuzi wa kisayansi wa masuala mbalimbali”. Alieleza Prof. Karimuribo.

Mkurugenzi wa Shahada za Juu Utafiti na Ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Karimuribo akitoa neno la ukaribisho

Akizungumzia madhumuni ya Warsha hiyo Mratibu wa Utafiti na machapisho kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema ni kuwajengea uwezo na mbinu Wanasayansi na Wanataaluma hao wachanga wa Chuo hicho kuweza kuandika maandiko yenye ushindani kwakuwa duniani ni ya ushindani hivyo lazima na wao waandike maandiko yenye kushinda ushindani huo.

“Hapa tunao Wanataaluma wetu wachanga ambao maandiko yao yameshinda kwenye mpango wa pili wa fedha za utafiti zinazotolewa na SUA kupitia SUARIS  hivyo kwenye warsha hii watajengewa uwezo zaidi wa namna kuboresha mawazo hayo kutoka kwenye wazo la awali na kuwa ndiko kamili.” Alifafanua Prof. Kashaigili.

Prof. Kashaigili amesema kwenye warsha hiyo wanatarajia washiriki watatambua kanuni za kutengeneza miradi na maandiko, Kuchambua matatizo na kuyafanyia kazi kwa mtiririko,kutengeneza mpango mzuri wa utekelezaji na kuandika maandiko yanayokidhi ushindani na bajeti zinazokidhi na kukubalika.

Mratibu wa Utafiti na machapisho kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya warsha na matarajio

Prof. Kashaigili amesisitiza kuwa Menejimenti inahitaji kuona Wanasayansi hao wanandika maandiko yenye kiini cha utafiti ili kuona Elimu ya utafiti ndani yake  na sio tuu maandiko ili kuweza kujibu changamoto mbalimbali katika jamii.

Mafunzo hayo ya siku nne  ya kuwajengea uwezo Wanasayansi na wanataaluma wachanga katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA yameendeshwa kwa ushrikiano katika ya SUA kupitia Kurugenzi yake ya Shahada za Juu utafiti na ushauri wa Kitaalmu pamoja na Mradi wa kujenga Vyuo vikuu imara (BSU)

Habari na Picha,
Calvin Gwabara

Share this page