Wanataaluma SUA wapokea mafunzo ya kuwajengea uwezo

Manajimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imepongeza jitihada zinazochukuliwa na Chama cha Wanataaluma SUA (SUASA) kwa kuwajengea uwezo Wanataaluma wake wachanga kupata mbinu na ujuzi wa kuandika maandiko yatayowasaidia kupata fedha za kufanya tafiti mbalimbali ambazo zinachangia katika kuwakuza kitaaluma.

SUA

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua mafunzo ya kujengea uwezo wanataaluma SUA ya namna ya kuandika Maandiko ya miradi ya tafiti lakini pia kupata ujuzi wa kuandika machapisho ya kisayansi.

Profesa Mwatawala aliwapongeza wawezeshaji wa mafunzo hayo ambao wengi ni wabobezi kwenye maeneo mbalimbali ya kitaaluma kwa kuamua na kukubali kutenga muda wao na kutoa, uzoefu, ujuzi na mbinu mbalimbali walizonazo kwa kizazi kipya cha wanataaluma wa SUA.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shahada za Juu, Utafiti, uhawilishaji wa teknolojia na ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Kalimuribo aliwataka wote walioshiriki tukio hilo kuzingatia mafunzo waliyopatiwa.
Alishukuru uongozi wa SUASA kwa kufanikisha mafunzo hayo muhimu ambayo yanakwenda kuwapa ujuzi na maarifa yatakayowasaidia katika kutafuta fedha za tafiti watakazozifanya kupitia maandiko mbalimbali duniani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa SUASA Sixbert Mourice ameeleza kuwa Chuo kina mkakati wa kuwawezesha watu wake kufanya tafiti kupitia mapato ya ndani ambapo imegundulika kwamba watu wengi wanakosa miradi hiyo kutokana na ushindani mkubwa wa maandiko yanayoandikwa.

“Tumeandaa mafunzo ya siku mbili ambayo lengo lake kuwajengea wezo wanataaluma hasa wale wanaoingia katika utumishi wa kitaaluma ili wapate uwezo waweze kushindania miradi kutoka kwa wafadhili mbalimbali ndani ya Chuo, nchini na nje ya nchi na tunatarajia kufanya hivyo tena kwasababu kwenye  mpango mkakati wetu tumepanga kuwa tutakuwa tukifanya mara mbili katika kila mwaka wa kitaaluma”, alisema Sixbert.

Imeandikwa na Amina Hezron na Calvin Gwabara – SUAMEDIA                               

 

Share this page