MAKISATU 2022: Serikali yaahidi kuendelea kuwekeza kwenye ubunifu nchini

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimedhamiria kujenga uwezo wa ndanI kwa kuendelea kuwekeza katika rasilimali Watu,Miundombinu na Vifaa vya kisasa vya Utafiti na Ubunifu pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za Sayansi na Teknolojia na sekta ya Viwanda ili kuchochea Ubunifu na Uvumbuzi nchini.

SUA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Othman Masoud akitoa hotuba yake ya ufunguzi

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Othman Masoud kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akizindua wiki ya kitaifa ya Ubunifu kwa mwaka 2022 Jijini Dodoma.

“Matunda ya jitihada hizo za Serikali katika utekelezaji wa malengo hayo na hatua zinazochukuliwa yote yanabainika kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) ambapo jumla ya Wabunifu 2,785 wameweza kuibuliwa mwaka huu na miongoni mwao wale walio mahiri zaidi ya 200 wameendelezwa na Serikali” alieleza Mhe. Masoud.

Amesitiza kuwa lengo kuu la Serikali ni kuwa Wabunifu na teknolojia zao walizozalisha ziweze kufikia hatua ya kupelekwa Sokoni na kutumika na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa Vijana na kuchangia pato la Taifa.

Mhe. Masoud amemesema katika kuhakikisha Ubunifu na Elimu ya Sayansi na Teknolojia inawekezwa kwa vijana ili kupata wataalamu wa fani mbalimbali kwa upande wa Zanzibar, tayari wameshaanzisha mradi wa kujenga vituo 22 vya Ubunifu wa Sayansi Unguja na Pemba ambavyo vimeanza kutumika na ni Mradi wenye thamani ya USD Milioni 35 zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza kuibua,kutambua na kuendeleza Ubunifu na Teknolojia hapa nchini na kuhamasisha matumizi yake katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi katika masuala ya Kijamii na Kiuchumi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanizbar Mhe. Othman Masoud kuhusu Panya wanavyoweza kutambua makohozi yenye TB sambamba na utambuzi wa mabomu

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua Maonesho hayo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda amesema maadhimisho hayo ya MAKISATU yanayofanyika kwenye Mikoa 16 ya Tanzania  ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu kama nyenzo ya kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na jamii.

“Wiki ya ubunifu ya kitaifa inahusisha Majukwaa,Majadiliano kuhusu maendeleo ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu nchini,mafunzo na Semina kwa Wabunifu ikiwemo elimu ya ujasiliamali aidha mijadala hiyo inawahusisha Watafiti,Wavumbuzi na Wabunifu na wadau mbalimbali wa Ubunifu na Serikali katika kuweka mikakati mbalimbali ya pamoja kuhamasisha matumizi ya Teknolojia na Ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii”alieleza Prof. Mkenda.

Mhe. Mkenda amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya mashindano hayo ya (MAKISATU) jumla ya Wabunifu 1785 wameibuliwa na kutambuliwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine na kwamba Wabunifu mahiri 200 wanaendelezwa na Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili Ubunifu wao ufikie hatua ya kuwa bidhaa na kuingia Sokoni na hivyo kuongeza fursa za ajira na kipato cha Vijana nchini ambapo tayari Bunifu 26 zimeingia Sokoni.

Amesema katika mashindano ya mwaka huu 2022 jumla ya Wabunifu 86 wamepatikana kutoka katika makundi yote nchi nzima  ili kushindanishwa na mwisho siku ya kilele wapatikana washindi ambao watatunukiwa zawadi na bunifu zao kuendelezwa na Serikali kupitia (COSTECH).

Akitoa neno la shukrani Muwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao ni ndio wafadhili wakuu wa (MAKISATU) Bi. Christine Musis amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kujenga utamaduni wa Ubunivu na Uvumbuzi nchini.

“Niko hapa kama mdau mkubwa wa Serikali katika kusaidia kuchochea Ubunifu kwa Vijana wa Kitanzania na kuwapa kianzio cha masaada wanaohitaji kupiga hatua kutoka mawazo,Sampuli kifani hadi kufikia hatua ya kufika Sokoni ili wawe injini ya ukuaji na maendeleo nchini Tanzania”alisisitiza Bi.Musis.

Awali kabla ya kufungua Wiki hiyo ya kitaifa ya Ubunifu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Othman Masoud na viongozi wengine wa Wizara na Serikali walitembelea mabanda mbalimbali yanayoonyesha Bunifu na Teknolojia mbalimbali ikiwemo banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na kuvutiwa na maelezo ya namna Panya wanavyoweza kutambua makohozi na mtu mwenye TB na kugundua mabomu maelezo yaliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Raphael Chibunda na baadae kupata maelezo kutoka kwa Prof. Gerald Misinzo  na kuona namna Gari ambalo ni maabara inayotembea(Mobile Lab) ya SUA ainavyofanya kazi.



Prof. Gerald Misinzo akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanizbar Mhe. Othman Masoud alipotembelea banda la SUA



Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Festo J. Dugange na Mkurugenzi wa Sayansi teknolojia na Ubunifu Prof. Maulilio Kipanyula wakipata maelezo ya namna Gari ambalo ni Maabara inayotembea inavyofanya kazi

Kuhusu MAKISATU

Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliasisiwa mwaka 2019 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Mashindano haya ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha na kuendeleza teknolojia na maarifa asilia ya ndani ili yaweze kuchangia katika uchumi wa nchi. MAKISATU yanafanyika kila mwaka na yanahusisha wabunifu kutoka makundi ya Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ufundi Stadi, Vyuo vya Kati, Vyuo Vikuu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo na Mfumo usio Rasmi.

Lengo la MAKISATU ni kuibua, kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza ubunifu wa Watanzania katika nyanja za Sayansi na Teknolojia ili kuchangia juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Matokeo tarajiwa ya MAKISATU ni kukua kwa hamasa ya ubunifu katika nyanja ya sayansi na teknolojia; matumizi ya sayansi, teknolojia, na ubunifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii; kuendeleza ubunifu ili kufikia hatua ya ubiasharishaji; kuchochea ugunduzi na ubunifu wa kisayansi na teknolojia

Habari na Picha : Calvin Gwabara - SUAMEDIA
 

Share this page