Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akihitimisha Maonesho ya Nanenane Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, alizitaka taasisi zinazohusika na tafiti kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kupata suluhisho la changamoto mbalimbali nchini, ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Katika kutekeleza agizo hilo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinaendelea kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Wafugaji Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, mradi huo wa miaka mitatu unaotekelezwa kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), unafanyika katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kijiji cha Mtanana, wilayani Kongwa, Dodoma.

Kiongozi wa mradi huo, Prof. Sebastian Chenyambuga, amesema mradi huo unalenga kutafuta suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa malisho inayochangia migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akisema wanachunguza aina mbalimbali za malisho yanayoweza kustahimili mazingira na kupatikana kwa muda mrefu wa mwaka, huku wakihamasisha wafugaji kuwa na idadi ya mifugo inayoendana na uwezo wa eneo la malisho.
Mfugaji Clement Alophonce, 55, kutoka Kijiji cha Mtanana, amesema awali haikuwa rahisi kwake kufikiria kupunguza idadi ya mifugo, lakini baada ya kuhamasishwa sasa amepunguza idadi ya mifugo.
“Niliamua kuuza ng’ombe zangu 56 wa kienyeji na kununua ng’ombe 14 wa kisasa, hiyo imenisaidia sigombani tena na wakulima,” amesema.
Kijiji cha Mtanana kina jumla ya wafugaji 1,320 wenye mifugo 7,829, hali inayofanya upatikanaji wa maeneo ya malisho kuwa changamoto kutokana na ufinyu wa ardhi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akieleza umuhimu wa mradi huo, Mkurugenzi wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema Tume hiyo imetoa shilingi milioni 400 kwa watafiti wa SUA baada ya kuwasilishwa kwa andiko la mradi huo, kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa suluhisho la migogoro ya wakulima na wafugaji na kuongeza tija katika uzalishaji wa nyama na maziwa yenye ubora na ushindani katika masoko ya kimataifa.
“Nimeona mabadiliko haya kuwa hayajabakia tu kwenye maandishi bali yameanza kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Juhudi za SUA na COSTECH zinaendelea kuunga mkono maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa na uwekezaji wa kimkakati katika kuongeza tija na ufanisi wa uzalishaji katika sekta ya mifugo.
