SUA Waandaa Sera ya Kudhibiti Unyanyasaji wa Kingono

Wataalamu na wadau wabobevu wa masuala Jinsia wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wamekutana kukamilisha rasimu ya  Sera ya chuo ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake katika kuelekea uanzishwaji wa  kitengo cha jinsia na hatimaye Dawati la Jinsia.

Sua Waandaa Sera ya Kudhibiti Unyanyasaji wa Kingono

Akieleza malengo ya kikao kazi hicho cha siku mbili Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye mradi wa wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) Prof. John Jeckoniah amesema kuwa ni kupitia rasimu hiyo ya Sera na Muongozo wake ili baadae uweze kuwasilishwa kwa uongozi wa Chuo kwa kuidhinishwa kupitia kwenye vikao vya maamuzi ya Chuo kupata Baraka na kuanza kutumika.

“Tumeona tuwakutanishe wataalamu hawa wa masuala ya Jinsia kutokana kuwa na uzoefu kutoka kwenye taasisi mbalimbali na Idara za Chuo chetu tuweze kuungalia na kuuboresha vizuri ili uweze kufaa na kutekelezeka kwenye chuo chetu na hivyo SUA kuwa na mazingira salama kwa kila mmoja anayetoa na kupata huduma wakiwemo Wahadhiri,Wafanyakazi waendeshaji,Wanafunzi pamoja na watoa huduma wengine chuoni kwetu” Alieleza Prof. Jeckoniah.

1 0

Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) Prof. John Jeckoniah akieleza malengo ya Kikao kazi hicho cha kupitia Rasimu hiyo.

Kiongozi wa masuala ya Jinsia kwenye mradi wa HEET amesema kazi ya utengenezaji wa rasimu ya  Sera ya Unyanyasaji na ukatili wa kijinsia (ikiwa ni pamoja na masuala ya ukatili wa Kingono) na muongozo wa utekelezaji wake ni sehemu ya utekelezaji wa muongozo wa Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kutaka kila Chuo kuwa na dawati la jinsia.

Aidha amesema kuwa kutokana na umuhimuwa wa jambo hilo wamefanikiwa kupata fedha kupitia mradi wa HEET na hivyo kusaidia kukamilisha kazi hiyo,Ununuzi wa vifaa kwaajili ya uanzishwaji wa kitengo cha jinsia na dawati la jinsia, kutoa elimu kwa wanajumuiya kwenye kampasi zote ili masuala hayo yaweze kueleweka vizuri kwa Chuo kizima na endapo  uongozi utaipitisha na kuanza kutumika  ili kuweka na kuwezesha mazingira salama kwa kujifunza na kufanya kazi kwa wadau wote wa chuo.

Prof. Jeckoniah amewataka wajumbe wa kikosi kazi hicho kushiriki kikamilifu kutoa mchango chanya na mapendekezo ambayo yatasaidia SUA kupata Sera nzuri zaidi ambayo itasaidia Chuo kuwa na mazingira salama kwa kila mmoja anapotoa na kupokea huduma.

IMG 9207

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu na kusikia malengo yake.

Akizungumzia safari toka mwanzo hadi kupatikana kwa rasimu ya sera hiyo na muongozo wake wa utekelezaji mtafiti na nguli wa masuala ya Jinsia Prof. Fatihiya Masawe amesema ilichochewa na Mradi mdogo wa maswala ya Unyanyasaji wa kingono ambao matokeo yake ilikuwa ni kupatikana kwa rasimu hiyo.

Amesema wakati wa uandaaji wa Sera hiyo walitembea kujifunza kwenye vyuo mbalimbali nchini kama vile Chuo kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi,DUCE, Chuo Kikuu cha Muhimbili na vyuo vingine  kuona namna wanavyoshughulika na masuala hayo na kukabiliana nayo.

IMG 9186

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu na kusikia malengo yake.

Prof. Fatihiya amebainisha kuwa pamoja na mambo mengi mazuri waliyojifunza kwenye maeneo waliyotembelea changamoto kubwa imekuwa ni utayari wa viongozi katika kutoa rasilimali ili kutekeleza Sera hiyo na hii inatokana na sera yenyewe kuwa mwiba mchungu kwa wanajumuiya wake wasiofuata maadili bora ya utendaji kazi kwa kutoa adhabu ambazo zinagusa maisha na ajira za wahusika.

“Ukiona wenye madaraka wanapata kigugumizi kuwepo kwa sera ya masuala hayo utajua kuwa kweli kuna changamoto lakini sera hii ni kifaa muhimu ambacho pia kinamsaidia kiongozi kuchukua hatua stahiki dhidi ya watenda makossa hayo na wanaotendewa na hii itawezekana kama utajengwa uelewa na kuwapa watu nafasi ya  kutoa taarifa za matendo hayo ili yakomeshwe” Alieleza Prof. Fatihiya.

2 0

Mtafiti nguli wa masuala ya Jinsia Prof. Fatihiya Masawe akiwasilisha rasimu hiyo ya sera ya chuo ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake kabla ya kuanza kujadiliwa.

Mbobevu huyo wa masuala ya Jinsia amesema Kuwepo kwa Sera hiyo sio tuu kutasaidia kuweka mazingira bora ya kazi na kujifunzia kwa wote kwenye taasisi bali kunawezesha kupatikana kwa miradi mbalimbali ya utafiti na maendeleo kwenye taasisi kwakuwa kuna baadhi ya wafadhili hawakubali kutoa ufadhili kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi ambazo hazina sera ya kudhibiti masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinisa ikiwa pamoja na ukatili wa kingono.

Changamoto na matukio ya unyanyasaji wa kingono yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kutoka kwenye vyuo mbalimbali na taasisi zingine na uwepo wa Sera na dawati mahususi kwaajili ya kushughulikia masula hayo kutasaidia kuongeza elimu na kupunguza matendo hayo na waathirika na kuleta usawa na usalama kwa jamii.

IMG 9186 1

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu na kusikia malengo yake.

 

3 0

Picha ya pamoja ya Baadhi ya washiriki wa kikosi kazi hicho cha kupitia rasimu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake.

Na: Calvin Gwabara – Kibaha.

Share this page