Washauri Masuala ya Jinsia Yafundishwe Kwenye Kozi Zote SUA

Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Mizengo Pinda wameushukuru Uongozi wa Chuo kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa kuwajengea uwezo wa kufahamu na namna ya kuingiza masuala ya Jinsia katika shughuli mbalimbali za Chuo.

Washauri Masuala ya Jinsia Yafundishwe Kwenye Kozi Zote SUA

Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani akitoa shukrani zake na neno la ufunguzi wa mafunzo hayo.

Akifungua mafunzo hayo Januari 9. 2023 Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi kimazoea kwa kuchukulia maswala ya jinsia kama swala la kawaida lakini kumbe ni jambo ambalo linawagusa katika kazi zao za kila siku.

“Mafunzo ya aina hii huwa hayapatikani kirahisi kama ambayo tumepata leo ni kwa siku moja lakini yamefungua uelewa wa watu wengi kuhusu maana na masuala mazima ya Jinsia na namna ya kuyatumia katika kazi zetu za kila siku na tunaomba mafunzo ya aina hii yaendelee maana kadri watu wanavyozidi kujengewa uwezo ndivyo wanavyozidi kudadisi na kuona njia bora za kutumia jinsia kwenye kazi zao za kila siku” alisema Prof. Katani.

Aidha Prof. Katani amependekeza maswala ya Jinsia kuangaliwa namna ya kuingizwa kwenye programu na kozi zinazotolewa na SUA na kuweza kufundishwa kama mada kwa wanafunzi wa kozi zote bila kujali wanasomea Misitu, Kilimo, Udaktari na zinginezo zote zinazotolewa SUA.

Aidha ameushukuru Mradi wa HEET na Wataalamu wa Jinsia waliofika kutoa mafunzo hayo na wanaamini mradi huo utaleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wake ili kuleta mafanikio zaidi kwa chuo.

Akieleza lengo la mafunzo hayo Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye Mradi wa  (HEET) Prof. John Jeckoniah amesema ni kuwajengea uwezo Wanataaluma, Waendeshaji na  Wanafunzi kufahamu na kuingiza maswala ya Jinsia katika shughuli zote muhimu za utendaji wa chuo jambo ambalo ni kwa mujibu wa miongozo ya chuo na Taifa.

2 (2)

Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye Mradi wa  (HEET) Prof. John Jeckoniah akieleza lengo na mafunzo hayo.

“Mafunzo haya ni muhimu sana maana yanawajengea uwezo Wanataaluma na Wanafunzi kutambua masuala ya Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanaweza kuwatokea katika mazingira yao ya kazi au ya masomo na jinsia ya kuchukua hatua au kutoa taarifa ili watu waliopewa dhamana ya kuyashughulikia waweze kuchukua hatua” alieleza Prof. Jeckoniah.

Kiongozi huyo wa masuala ya Jinsia amesema SUA ina Sera ya Jinsia, Rasimu ya sera ya kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambayo itakamilika hivi karibuni hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya kuwaandaa wadau hao muhimu katika utekelezaji wa uundwaji wa Dawati la Jinsia kwa mujibu wa maagizo ya Serikali ambayo yameelekeza vyuo vyote vya Elimu ya Kati na Juu kuwa na Dawati la Jinsia.

Prof. Jeckonia amefafanua Dawati la Jinsia ni mfumo rasmi ambao unawezesha Wafanyakazi, Wanafunzi na Wadau wengine wote wanaofanya kazi na chuo kuweza kutambua masuala ya kijinsia na namna ya kuyashughulikia na kwamba miongozo hiyo inakifanya Chuo kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia malengo mahususi kama ya chuo.

Kwa upande wake Makamu Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Anna Sikira amesema mafunzo hayo yatawasaidia sana namna ya kutengenza mazingira bora ya kusihi na kushirikiana kati ya Wafanyakazi, Wadau na  Wanafunzi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa wanaokuja kusoma hapo ni bado ni watoto wadogo wanahitaji malezi na uangalizi ili kuweza kufikia malengo yao.

IMG 0256

Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa kwenye mafunzo hayo.

“Wanafunzi wetu wengine ni wadogo sana na walipokuwa nyumbani na shule za Sekondari walikuwa na maisha ya kufungiwa na kulindwa sana lakinI wanapofika chuoni wanakuwa huru tukiamini ni watu wazima wenye zaidi ya miaka 18 hivyo wanahitaji bado uangalizi na elimu ya namna ya kuishi katika uhuru walionao kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni za chuo kwa hiyo mafunzo haya ni muhimu sana kwao na walimu wetu” alifafanua Prof. Sikira.

Amesema Dawati la Jinsia litasaidia kupokea masuala yote yanayohusu Jinsia maana sasa Wanajumuiya watakuwa wanajua sehemu husika ya kupeleka mambo hayo maana kwa upande wa Wanafunzi wanapeleka kwa mshauri wa wanafunzi na wengine hawapeleki kutokana na mazingira lakini dawati litakuwa sehemu salama na muhimu wa kushughulikia masuala hayo Chuoni.

 

4 (2)

Washiriki wa mafunzo hayo kutoka SUA Kampasi ya Mizengo Pinda iliyojumuisha Wanataaluma,Wanafunzi na Waendeshaji.

 Na: Calvin Gwabara - Katavi                       

Share this page